Mapema katika huduma ya Ndugu Branham ilikuwa wazi kwamba mfumo wa kimadhehebu uliundwa kuyaendeleza madhehebu ya kidini, wala si Injili ya kweli. Ndugu Branham aliiamini Biblia Neno kwa Neno, wala asingepatana, hata kama ilimaanisha kutengwa na wenzake, marafiki, ama familia.
Wakati angali akiwa ni mfuasi wa Kanisa la Kimishenari la Baptisti, aliombwa kuwaweka wakfu wahudumu wanawake. Hata hivyo, yeye alijua Maandiko vizuri sana. I Timotheo 2:12 inasema dhahiri, “Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume; bali awe katika utulivu,” na I Wakorintho 14:34 inasema, “Wanawake na wanyamaze katika makanisa, maana hawana ruhusa kunena…” Hii haikuwa ni kuwapinga wanawake, bali Biblia ilikuwa imeliandika dhahiri jambo hilo. Wakati mkataa ulipotolewa, yeye asingepatana kwa hiyo akaliacha kanisa hilo.
Hilo halikuwa ndilo Andiko la pekee lililopuuzwa na madhehebu. Bwana alimfunulia Ndugu Branham ukweli juu ya ubatizo. Yesu angewezaje kuagiza, “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu,” hata hivyo kila ubatizo uliorekodiwa katika Biblia ulikuwa ni katika Jina la Yesu? Mtume Petro aliagiza katika Matendo 2:38 kutubu na kubatizwa katika Jina la Yesu Kristo. Maandiko hutenda kazi katika umoja mkamilifu, bali ilihitaji nabii kuifunua siri hii: “Baba” si jina, “Mwana” si jina, na “Roho Mtakatifu” si jina. Ni kama tu vile mtu mmoja ni baba kwa watoto wake, mwana wa wazazi wake, na ndugu wa ndugu zake, hata hivyo jina lake si “baba,” “mwana,” wala “ndugu.” Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu ni sifa za Jina Lake Yesu Kristo. Mathayo 28:19 na Matendo 2:38 yamekuja kulingana kikamilifu.
Hata ile dhambi ya asili katika Bustani ya Edeni ilifunuliwa, sio kama kula tunda, bali ni jambo ovu zaidi. Je! kula kipande cha tunda kungewezaje kuwafunulia Adamu na Hawa mara moja kwamba walikuwa uchi? Kwa kweli haileti maana. Tofaa lina uhusiano gani na uchi? Nabii wa Mungu aliifunua siri hii wazi wazi.
Malaika walionenwa habari zao katika Ufunuo mlango wa 2 na wa 3 ni akina nani? Huenda majina yao yakasikika yanafahamika.
Wale wapanda farasi wa kisiri wa Ufunuo mlango wa 6 ni akina nani? Wana jambo moja shirika lililo muhimu sana.
Je! Marekani imetajwa katika Kitabu cha Ufunuo?
Wale 144,000 waliookolewa katika mlango wa 7 ni akina nani?
Yule kahaba mkuu wa mlango wa 17 ni nani? Utambulisho wake na siri hizi zote zilifunuliwa katika Ujumbe wa nabii huyu mkuu aliyetumwa kutoka kwa Mungu.
Si kwamba tu miujiza isiyohesabika ilimfuata mtu huyu, bali siri zilizofichwa katika Biblia katika nyakati zote pia zilifunuliwa katika huduma yake. Ilionekana wazi kwamba nabii huyu alitimiza Maandiko mengi zaidi mbali na Malaki 4.
Ufunuo 10:7: Isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.
Sauti inawalilia walimwengu watoke kwenye madhehebu na walirudie Neno asili la Mungu. Kila mmoja wetu ana nafasi ile ile waliyokuwa nayo Petro, Yakobo, na Yohana. Tuna nafasi ya kuhesabiwa pamoja na wachache wa Mungu walioteuliwa ambao wasingeyasujudia madhehebu ya kidini ya siku hizi.
Maandiko matakatifu yamenakili maisha na matendo ya watu waliotembea pamoja na Mungu na walikuwa wametiwa mafuta sana na Roho hata walitangaza BWANA ASEMA HIVI, nayo maneno yao yakathibitishwa kwa ishara na maajabu yasiyoweza kukosea. Walikuwa ni manabii wa Mungu, na Sauti ya Mungu kwa kizazi chao.
Je! nyakati ziko tofauti sasa na vile zilivyokuwa wakati Yesu alipokuwa hapa? Viongozi wa dini ndio waliomsulibisha. Wanafunzi walikuwa wachache mno miongoni mwa mfumo mkubwa sana wa kidini. Walitengwa, wakadhihakiwa, na hatimaye wakauawa kwa kuchukua msimamo dhidi ya mfumo wa madhehebu makubwa. Huenda tusiuawe kwa ajili ya imani zetu siku hizi, bali hakika tunateswa. Kama vile Mafarisayo na Masadukayo, wao hawawezi kuikana miujiza iliyoifuata huduma ya Ndugu Branham kwa hiyo wanakimbilia kufanya mashambulizi ya namna nyingine. Huenda ukasikia ya kwamba yeye alikuwa ni nabii wa uongo, kiongozi wa kundi lililojitenga, ama mabaya zaidi. Kwa kweli, yeye alikuwa ni mtu mnyenyekevu wa Mungu ambaye alisimama imara dhidi ya utawala wa kimabavu ambao madhehebu na vikundi vya dini yanao juu ya watu wa Mungu. Walimshambulia Yesu jinsi hiyo hiyo wakati Yeye alipopinga mafundisho yao ya sharti na mapokeo.
Mungu aliuheshimu msimamo wa Ndugu Branham wa kuamini kila Neno katika Biblia, Naye anaitumia huduma yake kuwaongoza mamilioni ya watu kwa Yesu Kristo. Leo hii, Sauti ya Malaika wa Saba inapiga baragumu kwa nguvu vile vile ilivyopata kuipiga. Kadiri ya watu milioni mbili ulimwenguni kote wanauamini Ujumbe wa Ndugu Branham. Huenda hii ikawa ni uchache mdogo sana wa watu bilioni mbili wanaokiri Ukristo, lakini je! ni wakati gani ambapo watu wa Mungu hawakuwa katika uchache?
Tuna zaidi ya jumbe 1,200 zilizorekodiwa zilizo na Sauti ambayo ilitabiriwa ingekuja katika Ufunuo 10:7. Kila moja ya jumbe hizi inafungua siri zaidi za Mungu. Sauti hiyo inapatikana kwa ajili yako kama unapenda kuisikia.
CHAGUO NI LAKO
Kamwe siwaletei watu ujumbe kusudi wanifuate, ama wajiunge na kanisa langu, ama waanzishe shirika na dhehebu fulani. Sijafanya hivyo kamwe wala sitafanya hivyo sasa. Sina haja ya mambo hayo, bali nina haja ya mambo ya Mungu pamoja na watu, na kama naweza kulitimiza jambo moja tu nitaridhika. Jambo hilo moja ni kuona uhusiano wa kweli wa kiroho baina ya Mungu na watu umeimarishwa, ambapo watu wanakuwa viumbe vipya katika Kristo, wamejazwa na Roho Wake na wanaishi kulingana na Neno Lake. Ningewaalika, ningewasihi na kuwaonya watu wote waisikie sauti Yake wakati huu, na kuyatoa maisha yenu kabisa Kwake, hata kama vile ninavyoamini moyoni mwangu kwamba nimeyatoa yangu yote Kwake. Mungu awabariki, na hebu kuja Kwake na kuifurahishe mioyo yenu.
Rev. William Marrion Branham
Kwa maelezo zaidi juu ya huduma ya Kasisi William Marrion Branham na jinsi ya kuzipata jumbe zake,
tafadhali wasiliana na:
THEMESSAGE.COM
P.O. Box 950
Jeffersonville, IN 47131, USA
812-256-1177