Mwanzo



“Nilipozaliwa katika kibanda kidogo cha Kentucky kule juu, Malaika wa Bwana aliingilia dirishani na kusimama pale. Kulikuwako na Nguzo ya Moto.”

Mapambazuko yalikuwa tu ndiyo kwanza yaanze kupenya giza la mbingu baridi za Aprili. Lile dirisha moja la mbao lilifunguliwa lipate kuiachilia nuru ya asubuhi iingie kwenye chumba hicho kidogo sana cha kibanda. Robini aliyesimama karibu na hilo dirisha alionekana amechangamka sana asubuhi hii na alikuwa akiimba kwa mapafu yake yote. Ndani ya kibanda hicho, kijana Charles Branham aliitia mikono yake kwenye ovaroli yake mpya kabisa na kuinama akimwangalia mke wake mwenye umri wa miaka 15. “Tutamwita jina lake William,” akasema baba yake.

Ndani ya hilo dirisha ikaja Nuru ya kimbinguni. Hiyo nuru ilijongea humo chumbani na kuning’inia juu ya kitanda ambapo huyo mtoto ndiyo kwanza azaliwe. Hii ilikuwa ni Nuru ile ile iliyowaleta wana wa Kiebrania kutoka Misri. Ilikuwa ni Nuru ile ile iliyokutana na Paulo akienda zake Dameski. Nayo itaenda kumwongoza mtoto huyu mdogo apate kumwita Bibi-arusi wa Kristo kutoka ulimwenguni. Hiyo Nuru haikuwa ni mwingine ila ni huyo Malaika wa Bwana, ile Nguzo ya Moto; na kwa mara nyingine tena ilikuwa imemtokea mwanadamu.

Na mle ndani, katika kibanda hiki kidogo cha mbao, asubuhi hiyo tarehe 6 Aprili, mkunga alifungua dirisha kusudi nuru iweze kuangazia ndani ili Mama na Baba waione sura yangu. Ndipo Nuru ya karibu ukubwa wa mto iliingia ikizungukazunguka upesi kupitia dirishani. Ilizungukazunguka mahali nilipokuwa, kisha ikashuka kitandani. Watu kadhaa wa mlimani walikuwa wamesimama pale. Walikuwa wakilia.

Makazi hayo duni yalikuwa katika milima ya Kentucky kusini, karibu na mji mdogo wa Burkesville. Ilikuwa ni tarehe 6 Aprili, 1909. Mtoto huyo mchanga alikuwa ndiye wa kwanza kati ya watoto kumi ambao wangezaliwa na Charles na Ella Branham.

Haikuchukua muda mrefu kabla ya Malaika wa Bwana kumtembelea mtoto William Branham tena.

Wakati alipokuwa mtoto mchanga, Malaika wa Bwana kwanza alisema naye, akisema ya kwamba angeyaishi maisha yake karibu na mji unaoitwa New Albany. Aliingia nyumbani na kumwambia mama yake yaliyokuwa yametukia tu. Kama mama yeyote, hakuitilia maanani hadithi hiyo naye akamweka kitandani apate kutuliza neva zake changa. Miaka miwili baadaye, familia yake ilihamia Jeffersonville Indiana, maili chache tu kutoka mji wa New Albany ulio kusini mwa Indiana.

Malaika alisema tena na huyo nabii kijana miaka michache baadaye. Ilikuwa ni siku tulivu ya Septemba huku jua lenye joto likiwaka kupitia kwenye matawi ya majira ya kupukutika. Mtoto huyo alikuwa akichechemea huku amebeba ndoo mbili za maji kupitia kwenye ujia. Gunzi la hindi lilikuwa limefungiwa chini ya kidole chake cha mguu kilichojeruhiwa kisije kikaingia uchafu. Aliketi chini ya mti mrefu wa mpopla apate kupumzika. Machozi yalikuwa yakitiririka kutoka machoni mwake huku akilia juu ya msiba wake: marafiki zake walikuwa wakijifurahisha kwenye shimo la mahali hapo la kuvulia samaki, naye alikuwa amekwama akimchotea baba yake maji. Mara, upepo ukaanza kuzungukazunguka juu yake mtini. Akapangusa macho yake na kusimama kwa miguu yake. Akasikia sauti ya majani yakichakarisha katika upepo…bali hakukuwa na upepo. Akaangalia juu, na yapata nusu ya urefu wa kwenda juu wa huo mpopla, kitu fulani kilikuwa kikizungushazungusha hayo majani yaliyokauka.

Mara Sauti ikanena, “Usinywe pombe wala kuvuta sigara wala kuuchafua mwili wako kwa njia yoyote, kutakuwako na kazi utakayofanya utakapokuwa mtu mzima.” Mvulana huyo aliyeingiwa na hofu mwenye umri wa miaka saba aliangusha ndoo zake akakimbilia kwa mamaye.

Kama vile nabii Samweli, Mungu alikuwa amezungumza na mtoto tena.

Majuma machache baadaye, alikuwa akicheza gololi na ndugu yake mdogo. Hisi ya ajabu ilimjia. Akaangalia huko kwenye Mto Ohio na kuona daraja zuri. Watu kumi na sita walianguka wakafa wakati hilo daraja lilipokuwa likivuka mto. Nabii kijana alikuwa ameona ono lake la kwanza. Alimwambia mama yake, naye akaandika simulizi lake. Miaka kadhaa baadaye, watu 16 walianguka wakafa wakati daraja la Mtaa wa Pili huko Louisville, Kentucky lilipokuwa likijengwa juu ya Mto Ohio.

Bwana alikuwa akimwonyesha maono ya usoni. Na kama vile manabii waliomtangulia, maono hayo hayakukosea kamwe.