Yafuatayao ni baadhi ya maswali ambayo tumepokea kuhusu huduma yetu. Endapo, baada ya kusoma haya, ungali una swali kuhusu yaliyomo kwenye tovuti hii, tafadhali tutumie barua pepe kwenye answers@themessage.com.

 

Kanuni yenu ya imani ni ipi?

Tungesema ya kwamba fundisho letu “rasmi” la kanisa ni Biblia, kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo. Kanuni yetu ya imani inaweza kuelezewa kifupi hivi: Hamna kanuni ya imani ila Kristo; hamna sheria ila upendo; hamna kitabu ila Biblia.

Mimi ni Mkristo tayari. Je! taarifa iliyo kwenye tovuti hii kweli ina faida kwangu?

Naam! Wakristo wanapaswa kuamini Neno lote la Mungu; hiyo ndiyo sababu tunaenda kanisani na kusoma Biblia zetu. Ni kwa nini uamini sehemu ya Biblia inayosema ya kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zako, na kupuuza jinsi dhambi ilivyoanza kwenye Bustani ya Edeni?

Ninaamini niliyosoma ni kweli. Nitajiunga namna gani?

Mwili wa Kristo si shirika wala dhehebu, na uanachama pekee unaohitajika ni kwamba umwamini Bwana Yesu. Usijali kuhusu kuwa na utambulisho wako ama kujaza makaratasi na uongozi wa kanisa. Amini tu Neno, naye Bwana atashughulikia yaliyosalia.

Je! ninyi ni kanisa?

Sisi si dhehebu la kanisa, bali tunayatumikia maelfu ya makanisa na mamilioni ya watu binafsi kote ulimwenguni kwa kuwapa vifaa vya kidini. Huduma yetu ni kuwahimiza watu kumkaribia Bwana Yesu kwa kuifanya Injili Yake ipatikane na kila mtu kwenye uso wa dunia.

Ninataka kubatizwa. Nini basi?

Endapo huwezi kumpata mtu yeyote wa kukubatiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, tutumie barua pepe pamoja na mahali ulipo nasi tutakutumia orodha ya makanisa katika eneo lako yanayoweza kukubatiza ifaavyo. Kumbuka, kulingana na Biblia ni muhimu kubatizwa katika Jina la Yesu, na si katika vyeo vya Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.

Je! mnafikiri nimepotea kwa kuwa mimi ni Mkatoliki ama mfuasi wa dhehebu lingine?

Bwana Yesu alisema, “Usihukumu, usije ukahukumiwa.” Hakuna mtu aliye na mamlaka ya kuamua wokovu. Yesu pia alisema, “Aaminiye na kubatizwa ataokolewa; lakini yeye asiyeamini atahukumiwa.” Kwa hiyo haijalishi kama wewe ni Mkatoliki, Mbaptisti, ama Mpentekoste; ukimwamini Bwana Yesu Kristo basi utaokolewa.

Voice Of God Recordings (VGR) ni nini?

Voice Of God Recordings, Inc. ni huduma inayohudumia madhehebu mbalimbali ambayo imejitolea kuendeleza Injili ya Bwana Yesu Kristo. Asili ya vifaa tunavyosambaza ni mahubiri yaliyorekodiwa ya hayati William Marrion Branham, nabii wa Mungu na mwinjilisti aliyetambulikana kimataifa. Vifaa vyetu ni pamoja na CD za MP3, DVD, Video, data, vitabu, magazeti, vitini, picha, vijarida, na tovuti.

William Branham ni nani, na ananihusu nini?

Kasisi Branham alikuwa mwinjilisti aliyejulikana kote ulimwenguni aliyekuwa kwenye huduma ya kimishenari kuanzia yapata 1947 hadi 1965. Si kwamba tu aliwaongoza mamilioni kwa Kristo, bali Mungu aliithibitisha huduma yake kwa miujiza isiyohesabika. Kiungo hiki kitakupa utangulizi wa huduma yake.

Kama miujiza hii yote kweli ilitendeka, inakuwaje sijapata kusikia habari zake?

Hilo ni swali zuri, na ambalo tungetaka kuyauliza makanisa yote makubwa leo. Mungu alimtuma nabii! Ni kwa nini kila mtu halizungumzii hilo? Wanapaswa kulizungumzia.

Ni kwa nini mnamtilia mkazo sana William Branham?

Kwa sababu ile ile ambayo Yoshua alimtilia mkazo Musa. Musa alikuwa nabii aliyeleta Ujumbe kutoka kwa Mungu. Ndugu Branham alifanya jambo lile lile.

Nimeona wanawake ambao wanahusika na huduma yenu. Ni kwa nini wote wana nywele ndefu na kuvaa sketi ndefu?

Paulo alisema katika I Wakorintho 11:15: “Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni fahari kwake: kwa sababu amepewa zile nywele ndefu ili ziwe badala ya mavazi.” Paulo pia alisema ya kwamba wanawake wanapaswa “kuvaa mavazi ya kujisetiri…” naye Musa alisema, “Mwanamke hatavaa mavazi yampasayo mwanamume.” Kama Biblia inasema hivyo, basi Wakristo wa kweli wataliamini.

Nilifanya utafiti mdogo nikapata tovuti kadhaa ambazo kazi yake ni kuyakanusha mambo aliyosema Kasisi Branham. Utawajibuje?

Utakutana na tovuti ambazo kazi yake ni kukanusha chochote na kila kitu, pamoja na Biblia. Tunakuomba tu ulinganishe Ujumbe tuliokuletea kwa Neno la Mungu, na sio kwa ushawishi ambao ni rahisi sana kuupata kwenye mtandao. Kumbuka, hakuna mtu aliyepata kukashifiwa zaidi ya Bwana Yesu. Kama unafanya mema, basi unaweza kutarajia kukosolewa.

Madhehebu yote yameingiza mikono yao mifukoni mwangu. Daima ni pesa.

Tambua kwamba hakuna mahali kwenye tovuti hii pa kutolea mchango. Ikifikia ambapo itatubidi kuomba fedha, basi wakati umewadia wa huduma hii kwisha. Hii haihusu pesa, inahusu kuwaleta watu kwa Yesu Kristo.

Ninataka kujifunza zaidi; hatua ya pili ni ipi?

Biblia inasema, ‘imani chanzo chake ni kusikia,” kwa hiyo tunakuhimiza uendelee kusikiliza. Tuna zaidi ya mahubiri 1,200 yaliyorekodiwa ambayo yaweza kupakuliwa bure. Tunaweza kukutumia vifaa kwa barua kama unapata shida kupakua faili za elektroniki.


www.branham.org hutuma habari za kila siku na shuhuda zinazohusu huduma yetu. Tunakualika kututembelea kila siku na kusoma taarifa kutoka kwa waaminio kote ulimwenguni. Huenda ukashangaa ni mambo mangapi makuu Bwana Yesu anafanya sasa hivi, katika siku hii ya kisasa.