Ni dhahiri, ubatizo ni muhimu sana, lakini je! Inajalisha tunabatizwa namna gani? Je! kuna ubatizo wa kweli, ama wowote ule utafaa? Kama unaiamini Biblia, basi NDIYO, kuna ubatizo wa kweli.
Karibu makanisa yote yanabatiza katika Jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, lakini jambo hili si sahihi kulingana na Biblia.
Katika Matendo 19, kulikuwako na watu fulani ambao tayari walimwamini Yesu Kristo, bali hawakuwa wamempokea Roho Mtakatifu mioyoni mwao. Mtume Paulo alijua njia inayofaa ya kumpokea Roho Mtakatifu, kwa hiyo akawauliza, “Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Nao wakasema, “Kwa ubatizo wa Yohana.” (Matendo 19:3) Paulo akaona ya kwamba hawakubatizwa kulingana na amri ya Petro katika Matendo 2:38, kwa hiyo akawaagiza wabatizwe tena katika Jina la Bwana Yesu. Ndipo, kama ilivyoahidiwa, wakampokea Roho Mtakatifu.
Kwa hiyo, ni kwa nini wanafunzi walibatiza katika Jina la Yesu wakati Yesu, Mwenyewe, aliwaambia wabatize katika Jina (sio “majina”) la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu? (Mat. 28:19) Je! walikosea? La! Walifanya vile hasa walivyoagizwa.
Unapoendelea kusoma makala haya, hebu wazia juu ya jina lako. Je! wewe ni mwana? Je! jina lako ni, “Mwana?” Je! wewe ni mama? Je! jina lako ni “Mama?” Bila shaka sivyo, hizo ni sifa tu. Unalo jina halisi, na vivyo hivyo na Mungu.
Hili hapa jibu:
Wala hakuna kitu kama mtu yeyote kubatizwa katika jina la Baba, Mwana, Roho Mtakatifu katika Biblia; kwa maana hakuna kitu kama hicho. Baba si jina; na Mwana si jina; na Roho Mtakatifu si jina; bali Jina la Baba, Mwana, Roho Mtakatifu ni Bwana Yesu Kristo.
Yesu Kristo ni Mungu! Yeye ni Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.
Kama unamtafuta Roho Mtakatifu na unashangaa ni kwa nini Bwana hajakupa bado, basi huenda ukataka kujiuliza swali lile lile ambalo Paulo aliuliza, “Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani?”
Marejeo
Mathayo 28:19
Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.
[Jina la Baba ni lipi? Jina la Mwana? Jina la Roho Mtakatifu?]
Marko 16:16
Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.
Yohana 5:43
Mimi nimekuja kwa Jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo.
[Kama Yeye anakuja kwa Jina la Baba Yake, basi Jina Lake ni lipi?]
Yohana 10:30
Mimi na Baba tu mmoja.
Yohana 12:45
Naye anitazamaye mimi anamtazama yeye aliyenipeleka.
Yohana 14:8-9
Filipo akajibu akamwambia, Utuonyeshe Baba, yatutosha.
Yesu akajibu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona Mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?
Yohana 20:27-28
Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.
Tomaso akajibu akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu.
Matendo 2:38-39
Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
Matendo 4:12
Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu lipasalo sisi kuokolewa kwalo.
Matendo 8:12
Lakini walipomwamini Filipo akihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.
Matendo 19:3-6
Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.
Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani Yesu.
Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
Na Paulo alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha na kutabiri.
Waefeso 4:5
Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.
Wakolosai 3:17
Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
I Yohana 5:7
Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu: nao hawa watatu ni mmoja.