Malaki 4:1

Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru…


Malaki 4:5-6

Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na kuogofya.
Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.


Kitabu cha mwisho cha Agano la Kale kinaahidi maangamizi ya ulimwengu. Bali kabla ya huo mwisho, nabii Eliya ameahidiwa kurudi na kumtambulisha Masihi. Wengine wanasema ya kwamba Yohana Mbatizaji aliutimiza unabii huu.

Miaka elfu mbili iliyopita, Wayahudi walikuwa wakimtarajia Masihi kuja. Walijua ya kwamba Malaki alitabiri mtu mwenye roho ya Eliya angemtambulisha Masihi kwao. Bali wakati Yohana Mbatizaji alipokuja, hakuwa kile walichomtarajia Eliya kuwa. Walipomswali Yesu ni kwa nini Eliya hakuwa amekuja kwanza, Yeye aliwaambia dhahiri ya kwamba Yohana alikuwa ndiye timizo la huo unabii: “Na kama mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja.”

Lilikuwa ni kundi dogo tu la watu lililoupokea ufunuo huu. Kwa viongozi wengi wa kidini, Yohana alikuwa si kitu ila mkosoaji wa madhehebu yao aliyezidi ulokole. Si kwamba tu hawakuitambua roho ya Eliya, bali baya zaidi, walikukosa kule Kuja kwa Kristo.

Basi je! Yohana Mbatizaji aliutimiza unabii wa Malaki? Sio wote.

Kwanza kabisa, ulimwengu bado “haujawaka kama tanuru,” kwa hiyo tunajua kwamba angalau sehemu ya Malaki 4 ingali haijatendeka. Sehemu nyingine ya Maandiko ambayo haikutimizwa na Yohana ilikuwa, “kuigeuza mioyo ya watoto iwaelekee baba zao.” Na, Yesu, Mwenyewe, alitabiri ya kwamba Eliya yuaja (wakati ujao) na atatengeneza mambo yote. (Matt 17:11)

Kwa hiyo tunapaswa kuwa tukimtarajia Eliya kabla ya kule Kuja kwa Kristo Mara ya Pili!

Sasa, katika siku hii ya kisasa, wakati wa Kuja kwa Bwana Yesu Mara ya Pili kumewadia. Tena, tumeahidiwa ya kwamba roho ya Eliya itamtambulisha Yeye kwetu kulingana na Malaki 4. Lakini ni kundi la watu wa aina gani litakalomtambua Eliya atakapokuja? Ni wale tu wanaomtarajia.

Tunayakumbuka maneno haya ya Bwana na Mwokozi wetu tunapowazia juu ya unabii wa Malaki kwa saa hizi za kuumalizia wakati:

Ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, nao hawakumtambua... Mathayo 17:12

Vipi kama tukikukosa huku kuja kwa Eliya? Je! tutakukosa basi kule Kuja kwa Kristo Mara ya Pili, kama vile waandishi na Mafarisayo walivyokukosa Kuja Kwake Mara ya Kwanza kwa kuwa hawakumtambua Yohana Mbatizaji?

 

 

 

 

Marejeo

II Wafalme 2:15

Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakamkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.

Isaya 40:3-4

Isikilizeni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya BWANA; nyosheni jangwani njia kwa Mungu wetu.

Kila bonde litainuliwa, na kila mlima na kilima kitashushwa; palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patasawazishwa. [Yohana Mbatizaji]

Malaki 3:1

Angalieni, namtuma mjumbe wangu [Yohana Mbatizaji], naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemtafuta, angalieni, anakuja, asema BWANA wa majeshi.

Malaki 4:1-6

Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru [halijatukia bado]; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema BWANA wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi.

Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawashukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kuchezacheza kama ndama wa mazizini.

Nanyi mtawakanyaga waovu; maana watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu, katika siku ile niifanyayo, asema BWANA wa majeshi.

Ikumbukeni torati ya Musa, mtumishi wangu, niliyomwamuru huko Horebu kwa ajili ya Israeli wote, naam, amri na hukumu.

Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na kuogofya.

Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao [Yohana Mbatizaji], na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao [Eliya wa siku hizi], ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.

Mathayo 11:10

Huyo ndiye aliyeandikiwa haya: Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeitengeneza njia yako mbele yako. [Malaki 3:1, Yohana Mbatizaji]

Mathayo 11:14

Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja. [Yohana Mbatizaji]

Mathayo 17:11-12

Yesu akawajibu akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza naye atatengeneza yote. [Eliya wa siku hizi]

Ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. [Yohana Mbatizaji] Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao.

Luka 1:17

Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa. [Yohana Mbatizaji]