Katika Biblia, Mungu daima aliuleta Ujumbe Wake kwa watu wa ulimwengu kupitia kwa nabii wa kizazi hicho. Yeye alisema na Musa kupitia kichaka kilichowaka moto na akampa agizo la kuwaongoza Waebrania kutoka Misri. Nguzo ya Moto iliyo dhahiri pamoja na ishara zingine zilitolewa kuthibitisha huduma yake. Yohana Mbatizaji alileta Ujumbe kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya kule kuja kwa Masihi. Wakati akimbatiza Bwana Yesu katika Mto Yordani, Sauti kutoka Mbinguni ililithibitisha agizo la Yohana la kumtambulisha Mwana-Kondoo wa Mungu, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa kukaa ndani Yake.” Miaka kadhaa baadaye, Sauti ya Bwana ilisikika tena ikizungumza na nabii wakati Yeye aliponena na Paulo kwa Nuru ya kupofusha, na baadaye akampa agizo la kuyaweka makanisa katika utaratibu. Kote katika Agano Jipya na la Kale, Mungu kamwe hajapata kuzungumza na watu Wake kupitia mfumo wa kimadhehebu ama shirika la kidini. Yeye daima amesema na watu kupitia mtu mmoja: nabii Wake. Naye aliwathibitisha manabii hawa kwa ishara za kimbinguni.
Lakini Je! ni vipi siku hizi? Je! Mungu angali analifunua Neno Lake kwa manabii? Je! kungali kuna ishara za kimbinguni? Je! Mungu angemtuma nabii wa siku hizi ulimwenguni? Jibu lake lililo dhahiri kabisa ni, “Ndiyo!”
Lakini tutajuaje wakati nabii atakapotokea? Je! ataonekanaje? Atafanya nini? Atatupa ishara gani? Atatimiza Maandiko gani?
Manabii wa kale walikuwa ni watu jasiri wa Mungu, wala hawakuhofu kukabiliana na mashirika ya kimadhehebu. Kusema kweli, karibu kila wakati walishutumiwa na makasisi. Eliya aliyapa changamoto mashirika ya kidini ya siku zake, akiwauliza kama Mungu angeiheshimu sadaka yao, ama yake. Walipiga makelele. Walitabiri. Wakaruka-ruka juu ya madhabahu hayo. Wakajikata-kata kwa visu. Bali Mungu hakuwasikia. Eliya aliangalia juu Mbinguni na kusema, “Na ijulikane leo ya kuwa Wewe Ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi Wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.” Ndipo basi akaagiza moto ushuke kutoka Mbinguni na kuiteketeza ile sadaka. Nabii Mikaya alishindana na Mfalme wa Israeli, na ukuhani wote, wakati alipomkemea Kuhani Mkuu Zedekia kwa kutabiri uongo. Huyo kuhani Mkuu alimchapa kofi usoni naye Mfalme akamfunga gerezani kwa kusema kweli. Hata Bwana Yesu alichukiwa sana na mashirika ya kidini ya siku Zake hata wakamsulibisha pamoja na wahalifu wabaya sana. Kama historia ikishikilia kuwa ni ya kweli, nabii angechukiwa na mfumo wa sasa wa kimadhehebu, naye angebandikwa jina la mzushi, nabii wa uongo, ama jina baya zaidi. Ila Mungu angemtetea mtumishi Wake.
Kama kulikuwako na nabii katika siku hizi za kisasa, angekubalikanaje na Kanisa Katoliki? Kanisa la Kibaptisti? Kanisa la Kilutheri? Dhehebu lo lote?
Bwana Yesu aliwaagiza wote wanaomwamini Yeye: “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; Kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; Watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” (Marko 16:17-18). Je! Andiko hili ni la kweli leo? Ikiwa si la kweli, je! Maneno ya Bwana yalikoma kutumika lini? Kote katika Biblia, manabii waliweza kuwaponya wagonjwa, kutoa pepo, na kufanya miujiza. Musa alimweka yule nyoka wa shaba mbele za watu wa Israeli kuwaponya wakiumwa na nyoka wa sumu (Hesabu 21:9). Naamani, Mshami hodari, alimjia Elisha apate kuponywa ukoma (II Wafalme 5:9). Wakati kijana mwanamume mmoja alipoanguka kutoka kwenye dirisha la juu akafa, mtume Paulo alimkumbatia na kuurejesha uhai kwenye mwili uliokufa (Matendo 20:10). Tuna taarifa ya kama miaka 3½ pekee ya maisha ya Bwana wetu Yesu, bali katika miaka hiyo michache, Yeye aliendelea kuwaponya wagonjwa. Vipofu walifanywa kuona. Wenye ukoma waliponywa. Viziwi walipokea kusikia kwao. Viwete walitembea. Kila namna ya ugonjwa iliponywa (Mat. 4:23).
Mungu pia aliwathibitisha manabii wake kwa njia zingine mbali na uponyaji. Hata siri zilizofichwa sana za moyo zilijulishwa watu hawa wa Mungu. Mfalme Nebukadreza alikuwa na ndoto iliyomsumbua, lakini asingeweza kukumbuka ilikuwa inahusu nini. Nabii Danieli alimfumbulia mfalme huyo ndoto hiyo pamoja na unabii uliofuata (Dan 2:28). Hakuna kitu alichofichwa Sulemani wakati Malkia wa Sheba alipokuja mbele zake. Yeye alikuwa amejazwa sana na Roho hata yeye alimpambanulia maswali ya moyoni mwake kabla hajayauliza (I Wafalme 10:3). Elisha alimfichulia Mfalme wa Israeli mipango yote ya Mfalme wa Shamu, hata maneno ya binafsi aliyonena katika chumba chake cha kulala (II Wafalme 6:12).
Kupitia matendo Yake mwenyewe, Bwana Yesu mara nyingi alionyesha ya kwamba Roho huyu wa utambuzi ni Roho wa Kristo. Yeye aliitambua tabia ya Nathanaeli wakati aliposema, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake!” Ndipo Yesu akaendelea kumwambia Nathanaeli mahali alipokuwa wakati Filipo alipomwambia kuhusu Masihi (Yohana 1:48). Wakati Nathanaeli alipoona ya kwamba Yesu aliujua moyo wake, papo hapo alimtambua kuwa Ndiye Kristo. Mara ya kwanza Yesu alipomwona Petro, alimwambia jina la baba yake, Yona (Yohana 1:42). Ndipo Petro alipoacha mambo yote na kumfuata Yesu maishani mwake mwote. Yesu alikutana na yule mwanamke Msamaria kisimani na kumwambia dhambi zake za wakati uliopita. Maneno yake ya kwanza yalikuwa, “Bwana, naona kwamba wewe u nabii” (Yohana 4:19). Watu wote hawa watatu walikuwa wametoka katika tabaka mbali mbali za maisha, hata hivyo walimtambua Yesu mara moja wakati alipoonyesha karama ya utambuzi.
Je! karama hii ilitoweka wakati ukurasa wa mwisho wa Biblia ulipoandikwa? Iwapo miujiza hii imeandikwa dhahiri jinsi hii katika Biblia, iko wapi siku hizi? Nabii wa siku hizi hakika angethibitishwa kwa miujiza.
Je! Mungu amewasahau watu Wake? Je! angali anaweza kuponya wagonjwa? Je! angali ananena nasi kupitia manabii Wake? Je! yeyote wa manabii hao alitangulia kuiona siku hii?
Je! kuna nabii ambazo hazijatimizwa bado?