Miaka Ya Ujana - Inaendelea



Kulianza kuingia giza zaidi kwenye chumba hicho cha hospitali, kana kwamba kilikuwa ni kwenye msitu mkubwa. Niliweza kusikia upepo ukivuma kupitia kwenye majani, hata hivyo ilionekana ni huko mbali sana mwituni. Huenda umesikia kishindo cha upepo ukivuma kwenye majani, ukizidi kukukaribia. Niliwaza, “Vema, hiki ni kifo kikija kunichukua.” Loo! nafsi yangu ilikuwa ikutane na Mungu, nilijaribu kuomba bali sikuweza.

Kadiri upepo ulivyosogea karibu, ndivyo ulivyozidi kutoa sauti kubwa. Majani yakatatarika na kwa ghafla, nikazimia.

IIlionekana basi kana kwamba nilirudia tena kuwa mvulana mdogo pekupeku, nimesimama kwenye ule ujia chini ya mti ule ule. Nikasikia sauti ile ile iliyosema, “Usinywe pombe kamwe wala kuvuta sigara.” Na majani niliyosikia yalikuwa ni yale yale yaliyovuma katika ule mti siku ile.

Lakini wakati huu ile Sauti ilisema, “Nilikuita nawe hukukubali kwenda.” Ikarudia kwa mara ya tatu.

Ndipo nikasema, “Bwana, kama huyo ni Wewe, nijalie nirudi tena duniani nami nitaihubiri Injili Yako hadharani na pembeni mwa barabara. Nitamwambia kila mtu habari zake!”

Wakati ono hili lilipopita, nilikuta ya kwamba sikuwa nimepata kujisikia vizuri zaidi. Daktari wangu mpasuaji alikuwa angali yumo humo jengoni. Alikuja na akaniangalia na akashangaa. Alionekana kana kwamba alifikiri ningekuwa nimekufa, ndipo akasema, “Mimi si mtu anayeenda kanisani, kazi yangu ni kubwa mno, bali ninajua Mungu amemzuru mvulana huyu.” Kwamba ni kwa nini yeye alisema hivyo, sijui mimi. Hakuna mtu aliyekuwa amesema jambo lolote kuhusu jambo hilo. Kama ningalikuwa nimejua wakati huo ninachojua sasa, ningalitoka kwenye kitanda hicho nikipaza sauti Sifa kwa Jina Lake.

Baada ya siku chache niliruhusiwa kurudi nyumbani, bali nilikuwa ningali mgonjwa na nililazimika kuvaa miwani machoni mwangu kwa sababu ya dosari katika jicho. Kichwa changu kilitikisika nilipoangalia kitu chochote kwa kitambo kidogo.

Nilianza kumwomba na kumtafuta Mungu. Nilienda toka kanisa moja hadi lingine, nikijaribu kupata mahali fulani ambapo palikuwa na wito wa madhabahuni wa mtindo wa kale. Jambo la kuhuzunisha lilikuwa kwamba sikuweza kupata popote.

Nilisema ya kwamba kama ningejaliwa kuwa Mkristo, kweli ningekuwa Mkristo hasa. Mhudumu aliyenisikia nikitoa tamshi hilo alisema, “Sasa Billy jamani, unaelekea kwenye ulokole.” Nikasema ya kwamba kama kamwe nikipata dini, nilitaka kuisikia wakati ikija, kama tu vile wanafunzi walivyofanya.

Loo Jina Lake lisifiwe. Nilipata dini baadaye kidogo na ningali ninayo, na kwa msaada Wake, nitaidumisha daima.

Usiku mmoja nilimwonea Mungu njaa sana na kuonea njaa tukio halisi hata nilitoka nikaenda nje nyuma ya nyumba kwenye kibanda cha zamani na kujaribu kuomba. Sikujua jinsi ya kuomba wakati huo kwa hiyo nilianza tu kuongea Naye kama vile ambavyo ningeongea na mtu yeyote yule. Mara kukatokea Nuru huko bandani na ikafanya msalaba na Sauti iliyotoka msalabani ikasema nami katika lugha ambayo sikuweza kuifahamu. Kisha ikaondoka ikaenda zake. Nilipigwa na bumbuazi. Nilipojirudia tena niliomba, “Bwana, kama huyo ni Wewe, naomba uje uzungumze nami tena.” Nilikuwa nikisoma Biblia yangu tangu niliporudi nyumbani toka hospitalini na nilikuwa nimesoma katika I Yohana 4, “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu.”

Nilijua ya kwamba roho fulani alikuwa amenitokea, na nilipoomba alitokea tena. Ndipo ilionekana kana kwamba kulikuwako na ratili elfu moja zilizonyanyuliwa toka kwenye nafsi yangu. Niliruka juu na kukimbilia nyumbani na ilionekana kana kwamba nilikuwa nikikimbia hewani.

Mama akauliza, “Bill, umepatwa na kitu gani?” Nikajibu, “Sijui bali kwa kweli ninajisikia vizuri na mwepesi.” Singeweza kukaa hapo nyumbani tena. Ilibidi nitoke nje na kutimua mbio.

Nilijua basi ya kwamba kama Mungu alinitaka nihubiri, angeniponya. Kwa hiyo nilienda kwenye kanisa lililoamini katika kupaka mafuta, nami nikaponywa papo hapo. Niliona basi ya kwamba wale wanafunzi walikuwa na kitu fulani ambacho wahudumu wengi sana siku hizi hawanacho. Wanafunzi walibatizwa na Roho Mtakatifu na kwa hiyo waliweza kuponya wagonjwa na kufanya miujiza mikuu katika Jina Lake. Kwa hiyo nikaanza kuomba kwa ajili ya ubatizo wa Roho Mtakatifu na nikaupata.

Siku moja yapata miezi sita baadaye, Mungu alinipa shauku ya moyo wangu. Alisema nami katika Nuru kuu, akiniambia niende nikahubiri na kuwaombea wagonjwa Naye angewaponya haidhuru walikuwa na ugonjwa wa namna gani. Nikaanza kuhubiri na kufanya yale ambayo aliniambia nifanye. Ee rafiki, siwezi kuanza kukwambia yale yote yaliyotendeka: Macho mapofu yalifumbuliwa. Viwete walitembea. Kansa zimeponywa, na kila namna ya miujiza imetendwa.

Siku moja mwishoni mwa Barabara ya Spring, Jeffersonville, Indiana, baada ya uamsho wa majuma mawili, nilikuwa nikibatiza watu 130. Ilikuwa ni siku yenye joto ya Agosti na kulikuwako na watu kama 3,000. Nilikuwa karibu na kumbatiza mtu wa 17 wakati mara moja niliisikia ile Sauti ndogo, tulivu tena na ikasema, “Angalia juu.” Mbingu zilikuwa kama shaba kwenye siku hiyo yenye joto ya Agosti. Hatukuwa na mvua kwa yapata majuma matatu. Niliisikia Sauti hiyo tena, na halafu tena mara ya tatu ikasema, “Angalia juu.”

Nikaangalia juu na nyota kubwa inayoangaza ikashuka kutoka mbinguni, ambayo nilikuwa nimeiona mara nyingi hapo kabla bali sikuwa nimewaambia habari zake. Mara nyingi nimewaambia watu juu ya kuonekana kwake nao wangecheka tu na kusema, “Bill, unawazia tu hayo. Ama labda ulikuwa unaota.” Lakini Mungu asifiwe, wakati huu alikuwa amejionyesha wazi kwa wote, kwa sababu ilikuja karibu sana nami hata sikuweza kuzungumza. Baada ya sekunde chache kupita nilipaza sauti na watu wengi wakaangalia juu na kuiona hiyo nyota juu yangu kabisa. Wengine walizimia wakati wengine wakipiga makelele na wengine wakakimbia. Ndipo hiyo nyota ikarudi mbinguni na mahali ilipokuwa imeondoka palikuwa ni futi kumi na tano mraba na mahali hapa pakaendelea kusogea na kuvurugika ama kana kwamba mawimbi yalikuwa yakifingirika. Mahali hapa palikuwa pamefanya wingu dogo jeupe na hiyo nyota ilitwaliwa juu katika wingu hili dogo.

Kama vile Yohana Mbatizaji, nabii huyu alithibitishwa kwenye maji ya Ubatizo.