Miaka Ya Ujana



Kote katika maisha yake, Ndugu Branham alitamani kuwa nyikani. Kwenye umri wa miaka 18, aliondoka Indiana kwenda kwenye milima ya magengemagenge ya magharibi. Kukaa kwake Arizona hakukuchukua muda mrefu kabla ya kulazimika kurudi.

Siku moja niliamua ya kwamba nilikuwa nimepata njia ya kuondolea mbali wito huo. Nilikuwa ninakwenda magharibi kufanya kazi kwenye ranchi. Ewe rafiki, Mungu ni mkuu tu huko nje kama alivyo mahali popote. Naomba ufaidike na uzoefu wa maisha yangu. Anapokuita, mjibu.

Asubuhi moja ya Septemba katika mwaka wa 1927, nilimwambia mama yangu ya kwamba nilikuwa ninaenda kwenye ziara ya kupiga kambi huko Tunnel Mill, ambako ni kama maili kumi na nne kutoka Jeffersonville tulikoishi wakati huo. Nilikuwa tayari nimepanga safari ya Arizona pamoja na marafiki fulani. Wakati mama aliposikia kutoka kwangu tena, sikuwa Tunnel Mill bali Phoenix, Arizona, nikimkimbia Mungu wa Upendo. Maisha ya ranchi yalikuwa ni mazuri sana kwa muda, lakini mara yalichujuka, kama ilivyo kwa anasa nyingine yoyote ya ulimwenguni. Ila hebu niseme hapa, Mungu Asifiwe, ya kwamba uhusiano wa maisha na Yesu unazidi kuwa mtamu na mtamu wakati wote wala hauchujuki. Yesu huleta amani kamilifu na faraja siku zote.

Mara nyingi nimesikia upepo ukivuma katika misonobari mirefu. Ilionekana kana kwamba ningeweza kusikia sauti Yake ikiita huko mwituni, ikisema, “Adamu, uko wapi?” Nyota zilionekana zikiwa karibu sana mtu ungaliweza kuzichuma kwa mikono yako. Mungu alionekana kuwa yuko karibu sana.

Jambo moja kuhusu nchi hiyo ni zile barabara jangwani. Mtu ukitoka kwenye barabara, unapotea kwa urahisi. Mara nyingi sana watalii wanaona maua madogo ya jangwani na wanaondoka kwenye barabara kuu kwenda kuyachuma. Wanazurura jangwani na wanapotea na mara nyingine wanakufa kwa kiu. Ndivyo ilivyo katika njia ya Mkristo — Mungu ana njia kuu. Anazungumza juu yake katika Isaya, mlango wa 35. Inaitwa “Njia Kuu ya Utakatifu.” Mara nyingi anasa ndogo za ulimwengu zinakuvuta kukutoa kwenye njia kuu. Ndipo umepoteza mawasiliano yako na Mungu. Jangwani wakati mtu umepotea, mara nyingine kunatokea mazigazi. Kwa wale watu wanaokufa kwa kiu, mazigazi hayo yatakuwa ni mto ama ziwa. Mara nyingi watu huyakimbilia na kutumbukia ndani yao ndipo tu wanakuta kwamba wanaogelea tu kwenye mchanga wenye joto. Wakati mwingine ibilisi anakuonyesha jambo fulani ambalo anasema ni wakati wa kujifurahisha. Hayo ni mazigazi tu, ni kitu ambacho si halisi. Ukisikiliza utajikuta tu ukijilundikia huzuni nyingi kichwani mwako. Usimsikilize, mpendwa msomaji. Mwamini Yesu awapaye maji yaliyo hai hao wenye njaa na kiu.

Siku moja nilipata barua kutoka nyumbani ikisema ya kwamba mmoja wa ndugu zangu alikuwa ni mgonjwa sana. Ilikuwa ni Edward, aliyenifuata kwa umri. Hakika nilifikiri haukuwa mbaya sana, kwa hiyo niliamini atapona. Walakini, jioni moja siku chache baadaye nilipokuwa nikirudi kutoka mjini kupitia kwenye bwalo la chakula kwenye ranchi, niliona karatasi mezani. Nikaichukua. Ilisema, “Bill, njoo huku kwenye malisho ya kaskazini. Muhimu sana.” Baada ya kuisoma mimi pamoja na rafiki yangu tulienda kwenye malisho hayo. Mtu wa kwanza niliyekutana naye alikuwa ni maskini Mteksasi aliyefanya kazi kwenye ranchi hiyo. Jina lake lilikuwa ni Durfy, bali tulimwita “Pop.” Alikuwa na uso wenye huzuni aliposema, “Billy, jamani, nina habari za kuhuzunisha kwako.” Wakati uo huo mnyapara akaja akitembea. Wakaniambia ya kwamba barua ya simu ilikuwa ndiyo kwanza ifike, ikiniambia kuhusu kifo cha ndugu yangu.

Rafiki mpendwa, kwa muda kidogo nisingeweza kusogea. Yalikuwa ndiyo mauti ya kwanza nyumbani mwetu. Ila ninataka kusema ya kwamba jambo la kwanza nililowazia lilikuwa kama alikuwa tayari kufa. Nilipogeuka na kuangalia mbuga hiyo pana ya majani ya manjano, machozi yalitiririka mashavuni mwangu. Jinsi nilikumbuka vile tulivyopambana kwa pamoja tulipokuwa watoto wadogo na jinsi tulivyopata shida nyingi.

Tulienda shuleni bila chakula cha kutosha. Vidole vya miguu vilikuwa vimetokeza kwenye viatu vyetu na ilitulazimu kuvaa makoti yaliyochakaa yaliyofungwa shingoni kwa pini kwa kuwa hatukuwa na mashati. Jinsi nilivyokumbuka pia ya kwamba siku moja mama alikuwa ameweka bisi kidogo katika ndoo ndogo kwa ajili ya chakula chetu cha mchana. Hatukula pamoja na watoto wengine. Tusingeweza kupata chakula kama walichokuwa nacho. Daima tungechurupukia kilimani tupate kula. Ninakumbuka hiyo siku tulipokuwa na bisi, tulifikiri ilikuwa ni tafrija hasa. Kwa hiyo ili kuhakikisha nilipata fungu langu la hizo, nilitoka kabla ya adhuhuri na kuchota konzi nzima kabla ndugu yangu hajapata fungu lake.

Basi nikisimama hapo nikiangalia mbuga pana iliyokaushwa na jua niliwazia juu ya mambo hayo yote na kujiuliza iwapo Mungu alikuwa amempeleka mahali bora zaidi. Ndipo tena Mungu aliniita, lakini kama kawaida, nilijaribu kuupiga vita.

Nilijiandaa kuja nyumbani kwa ajili ya mazishi. Wakati Kasisi McKinney wa Kanisa la Port Fulton, mtu ambaye ni kama tu baba kwangu mimi, alipohubiri mazishi yake, alitamka ya kwamba “Huenda ikawa kuna wengine hapa wasiomjua Mungu, kama wapo, mkubalini sasa.” Loo, jinsi nilivyoshikilia kiti changu. Mungu alikuwa akinishughulikia tena. Msomaji mpendwa, Yeye anapoita, mwitikie.

Sitasahau kamwe jinsi ambavyo maskini Baba yangu na Mama walivyolia baada ya yale mazishi. Nilitaka kurudi Magharibi bali Mama alinisihi sana nikae hata hatimaye nikakubali kukaa kama ningaliweza kupata ajira. Mara nikapata ajira kwenye Kampuni ya Utumishi wa Umma ya Indiana.

Yapata miaka miwili baadaye nilipokuwa nikipima mita katika duka la mita kwenye Mtambo wa Gesi huko New Albany, nililemewa na gesi na kwa majuma kadhaa niliteseka kutokana nayo. Niliwaendea madaktari wote niliowajua. Sikuweza kupata nafuu. Niliumwa na tumbo lenye asidi, iliyosababishwa na athari ya gesi. Hali ilizidi kuwa mbaya wakati wote. Nilipelekwa kwa wataalamu huko Louisville, Kentucky. Hatimaye walisema ni kidole tumbo changu na wakasema ilibidi nifanyiwe upasuaji. Sikuweza kuamini jambo hilo kwa kuwa kamwe sikuwa na maumivu ndani ya ubavu wangu. Madaktari walisema wasingeweza kunifanyia jambo lingine lolote mpaka nifanyiwe upasuaji. Hatimaye nilikubali ufanywe bali nilisisitiza ya kwamba watumie nusukaputi ya kawaida ili kwamba niweze kuufuatilia huo upasuaji.

Loo, nilitaka mtu fulani asimame kando yangu ambaye alimjua Mungu. Niliamini katika maombi bali sikuweza kuomba. Kwa hiyo mhudumu kutoka kwenye Kanisa la Kwanza la Kibaptisti aliambatana nami kwenye chumba cha kufanyiwa upasuaji.

Waliponichukua kutoka mezani wakanipeleka kwenye kitanda changu, nilijisikia nikiendelea kuwa dhaifu zaidi na zaidi wakati wote. Moyo wangu ulikuwa ukidunda kwa shida. Nilihisi kifo kikiwa juu yangu. Kupumua kwangu kulikuwa kukipungua wakati wote. Nilijua nilikuwa nimefikia mwisho wa safari yangu. Ewe rafiki, ngoja mpaka utakapofika hapo wakati mmoja, ndipo utakapofikiria juu ya mambo mengi uliyofanya. Nilijua kamwe sikuwahi kuvuta sigara, kunywa pombe, wala kuwa na tabia zozote chafu bali nilijua sikuwa tayari kukutana na Mungu wangu.

Ewe rafiki yangu, kama wewe ni mfuasi baridi na wa kawaida tu wa kanisa, utajua wakati utakapofika mwisho ya kwamba huko tayari. Kwa hiyo kama hayo tu ndiyo unayojua kumhusu Mungu wangu, ninakuomba papa hapa upige magoti na kumwomba Yesu akupe tukio lile la kuzaliwa mara ya pili, kama vile alivyomwambia Nikodemo katika Yohana mlango wa 3, na loo, jinsi ambavyo kengele za furaha zitakavyolia. Jina Lake na lisifiwe.