Maneno ya mwisho kabisa yaliyoandikwa katika Agano la Kale yanatoa ahadi hii: “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na ya kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.” (Mal 4:5-6)
Siku ya Bwana iliyo kuu na ya kuogofya haijakuja bado, kwa hiyo inatupasa kumtazamia nabii Eliya kwa moyo. Katika Biblia, manabii hawakuyajilia madhehebu makubwa ya kidini. Waliwajilia wachache waliochaguliwa. Wazia kama yule nabii wa Malaki 4 angelikuja, asitambulikane. Vipi kama yeye ni kama wale manabii wa kale, na ni watu wachache tu wanaomtambua? Kama nabii huyu atarudi katika siku za mwisho, tutamjuaje? Jibu lake linaonekana dhahiri katika Maandiko. Yeye atakuwa na tabia ya nabii. Atazijua siri za moyo. Atafanya miujiza. Madhehebu ya kidini yatajaribu kumkosoa. Bali kutakuwako na wachache waliochaguliwa ambao watamtambua kama mjumbe aliyeahidiwa kwa ajili ya siku hizi.
Tutajuaje wakati Eliya atakaporudi? Yeye ataonyesha tabia zipi kusudi tuweze kumtambua?
Eliya alikuwa ni mtu wa nyikani. Ishara kuu na maajabu yaliifuata huduma yake. Alihubiri dhidi ya maovu ya siku zake. Zaidi sana alihubiri dhidi ya utovu wa uadilifu wa Malkia Yezebeli. Wakati Eliya alipotwaliwa juu Mbinguni katika gari la moto, roho yake ilishuka juu ya Elisha. Ndipo ishara kuu na maajabu yakaifuata huduma ya Elisha, naye pia alihubiri dhidi ya dhambi za ulimwengu. Manabii hao wote wawili walisimama peke yao dhidi ya mashirika ya kidini ya siku hizo. Mamia ya miaka baadaye, roho yule yule alirudi duniani katika Yohana Mbatizaji. Nabii Malaki alibashiri ya kwamba Eliya angerudi kumtambulisha Bwana: “Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu...” (Malaki 3:1). Yohana Mbatizaji alitimiza hayo wakati akihubiri toba miongoni mwa watoto wa Mungu. Kama vile Eliya, yeye alihubiri dhidi ya mfalme na madhehebu ya kidini ya siku hizo. Bwana Yesu alithibitisha ya kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa ndiye nabii wa Malaki 3 katika Kitabu cha Mathayo (11:10): “Huyu ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeitengeneza njia yako mbele yako.” Luka 1:17 inasema ya kwamba roho ya Eliya (Elias) ilikuwa iwe katika Yohana Mbatizaji, “Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto.” Lakini angalia kwamba sehemu ya pili ya Malaki 4 ilikuwa bado haijatimizwa: “…na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.” Sehemu hiyo ya Maandiko itatimia kabla ya kuja kwa Kristo Mara ya Pili.
Miaka elfu mbili baada ya Yohana Mbatizaji, wakati umewadia tena kwa roho ya Eliya kurudi duniani.
Siku hiyo imewadia! Katika wakati huu, tumeiona roho ya Eliya ikirudi. Yeye aliupinga mfumo wa madhehebu ya kisasa. Alizikemea dhambi za ulimwengu. Alionyesha ishara na maajabu yasiyohesabika. Aliihubiri Biblia neno-kwa-neno kutoka Mwanzo hadi Ufunuo. Nabii wa Malaki 4 alikuja kama ilivyoahidiwa, naye akaleta Ujumbe kutoka kwenye Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu. Jina la nabii huyo ni William Marrion Branham. Sisi tunamwita “Ndugu Branham.”
“William Branham, niliyempenda na kuamini yeye ni nabii wa Mungu.”
Oral Roberts, mwinjilisti anayejulikana sana ulimwenguni na mwanzilishi wa Chuo Kikuu cha Oral Roberts.
“William Branham alikuja kwetu kama nabii wa Mungu na akatuonyesha katika karne ya ishirini vitu vile vile dhahiri ambavyo vilionyeshwa katika Injili…Mungu amewatembelea watu Wake, kwa kuwa nabii mkuu ameinuka miongoni mwetu.”
Dr. T.L. Osborn, mwinjilisti wa Kipentekoste na mwandishi hodari.
“Kabla ya kumwombea mtu, angetoa utondoti sahihi kuhusu maradhi ya mtu huyo, na pia utondoti wa maisha yao - mji wanamoishi, kazi, matendo-hata huko nyuma kabisa utotoni mwao. Branham kamwe hakufanya makosa hata mara moja akiwa na neno la maarifa katika miaka yote niliyokuwa pamoja naye. Hiyo inajumuisha, kwangu mimi, maelfu ya visa.”
Ern Baxter, mwinjilisti, meneja wa Miamsho ya Branham kwa muda wa miaka saba, pia mmoja wa viongozi wa mwanzoni wa Huduma Mpya ya Kanisa la Kiingereza.
Hakuna mtu ambaye ameugusa ulimwengu kwa undani hivyo tangu Bwana Yesu Kristo alipotembea duniani. Kutoka kwenye asili duni katika kibanda cha chumba kimoja kwenye milima ya Kentucky, hadi Amarillo Texas ambako Bwana alimchukua Nyumbani, maisha yake daima yalijaa matukio ya mambo ya kimbinguni. Kwa kuongozwa na Malaika wa Bwana katika mwaka wa 1946, huduma ya Ndugu Branham ilitoa cheche iliyowasha kipindi cha ufufuo mkuu wa uponyaji ulioenea Marekani upesi na kote ulimwenguni. Hata siku ya leo, yeye anatambuliwa na wanahistoria Wakristo kama “baba” na “kiongozi” wa ufufuo wa uponyaji wa miaka ya 1950 ambao ulilibadilisha Kanisa la Kipentekoste na hatimaye ukaizaa huduma ya Karisma, ambayo siku hizi inashawishi karibu kila dhehebu la Kiprotestanti. Hata hivyo, kama ilivyo kawaida yao, madhehebu yanayapuuza mafundisho yake na kulikana agizo lake.
Popote alipoenda, Mungu alithibitisha ya kwamba Ndugu Branham ndiye nabii wa kizazi hiki. Kama vile Ayubu, Bwana alisema naye katika upepo wa kisulisuli. Kama vile Musa, Nguzo ya Moto ilionekana ikimwongoza. Kama vile Mikaya, alishutumiwa na makasisi. Kama vile Eliya, yeye alikuwa ni mtu wa nyikani. Kama Yeremia, aliagizwa na Malaika. Kama Danieli, yeye aliona maono ya usoni. Kama Bwana Yesu, alijua siri za moyo. Na kama vile Paulo, yeye aliwaponya wagonjwa.
Bwana amewatembelea watu Wake tena kupitia nabii. Katika wakati wenye giza sana wa historia, ambapo uadilifu umezama kwenye viwango ambavyo kamwe havijaonekana katika siku za nyuma na silaha za maangamizi ya hadhara zikitishia kwenye upeo wa macho, mtu mnyenyekevu alitumwa kutoka kwenye uwepo wa Mungu kuialika jamii inayokufa ipate kutubu.
Mwanafunzi mpendwa Yohana aliandika kuhusu Bwana Yesu:
Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa. Amina. (Yohana 21:25).
Jambo lilo hilo linaweza kusemwa kuhusu maisha ya Ndugu Branham. Kuna zaidi ya jumbe 1,200 zilizorekodiwa pamoja na maelfu ya hadithi zinazohusu maisha ya mtu huyu hodari. Hata sasa tunaendelea kusikia shuhuda mpya za ushawishi wake juu ya maisha ya mamilioni ya watu. Kijitabu hiki kisingeweza kubabia ushawishi ambao mtu huyu wa Mungu alikuwa nao juu ya ulimwengu.