Yohana 5:28-29

Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote walio makaburini wataisikia sauti yake.
Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima; na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.


Siku yaja ambapo kila mmoja wetu, kama ni Mkristo ama vinginevyo, atajua kile hasa kilicho ng’ambo ya pazia la wakati. Biblia inaahidi Uzima wa Milele kwa baadhi, na hao wengine, inaahidi hukumu. Kila mwanadamu kote katika historia hakika amejiuliza mwenyewe, “Itakuwaje kwangu nitakapokufa?”

Zamani za kale kabla hapajakuwapo na Biblia ya kusoma, nabii Ayubu aliangalia maumbile. Alinena kuhusu matumaini ya mti, jinsi ambavyo ungekatwa uanguke na kufa, hata hivyo kupitia kwa harufu ya maji, unachipuka na kuishi tena na kuchipusha matumba mapya. Ayubu alijua ya kwamba mwanadamu, kama vile mti, angefufuka tena:

Mtu akifa, je! atakuwa hai tena? Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, hata kufunguliwa kwangu kunifikilie.

Wewe ungeita, nami ningekujibu; ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako.

Lakini sasa wazihesabu hatua zangu; Je! huchungulii dhambi yangu? (Ayubu 14:14-16)

Huenda Ayubu hakuwa na Biblia ya kusoma, bali yeye alijua ya kwamba Mungu siku moja angemfufua kutoka kaburini wakati Mkombozi wa jamii ya wanadamu atakapokuja.

Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni!

Yakachorwa katika mwamba milele, kwa kalamu ya chuma na risasi.

Lakini mimi ninajua ya kuwa mkombozi wangu yu hai. Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.

Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, bado nikiwa na mwili wangu nitamwona Mungu. (Ayubu 19:23-26)

Nabii huyu alikuwa akinena juu ya Bwana Yesu na ufufuo wa watu Wake. Kwa ufunuo Ayubu alijua ya kwamba ingawa miili yetu huenda ikanyauka kabisa, Yesu atairejesha miili yetu. Na kwa macho yetu wenyewe, tutakuona kule Kuja Kwake. Watu wote wa Mungu wanatamani kuiona siku hiyo yenye utukufu.

Hata hivyo, kwa hakika tu kama Mungu alivyo hai, pia kuna ibilisi; na kwa hakika tu kama kulivyo na Mbingu, pia kuna jehanamu. Thawabu ni kubwa zaidi ya tunavyoweza kuwazia. Mtume Paulo alisema ya kwamba, “Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.” (I Kor. 2:9)

Akili zetu haziwezi kufahamu jinsi Mbinguni kutakavyokuwa kuzuri, wala haziwezi kufahamu vitisho vya jehanamu. Yesu alitwambia ya kwamba jehanamu ni kubaya sana hata ingekuwa ni afadhali kama tukikatilia mbali sehemu ya mwili wetu kuliko kujihatarisha kwenda mahali hapo pa kutisha mno.

Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanamu, kwenye moto usiozimika. (Marko 9:43)

Kwa hiyo ni nani atakayeenda Mbinguni? Na ni nani atakayeenda jehanamu? Ni wazo la kuhuzunisha, bali Yesu alisema kuwa watu wengi hawatapokea zawadi anayotaka kuwapa: Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache. (Mat. 7:13-14)

Yesu pia alisema, “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” (Mat. 7:21-23)

Kwamba tu mtu anadai Ukristo haimaanishi ya kwamba ameokoka. Kwa hiyo, hili ndilo swali dhahiri mioyoni mwetu: Je! ninaupokeaje Uzima wa Milele? Yesu alitupa jibu rahisi sana: Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. (Yohana 5:24)

Jambo la kusikitisha ni kwamba, kuna watu wachache sana duniani siku hizi ambao wako tayari kuchukua wakati kutoka kwenye siku zao zenye shughuli nyingi kulisikia Neno la Mungu. Na hata ni wachache zaidi ambao wataliamini Neno wakiisha kulisikia.

Makanisa yanatwambia tuwe mtu mzuri, tuwazie mema, tusidanganye, kusema uongo, wala kuiba, nasi tutaenda mbinguni. Hawaelewi ya kwamba jehanamu itajaa watu wanaoonekana kuishi maisha mazuri. Ukweli ni kwamba hatutaenda Mbinguni kwa sababu ya matendo yetu mazuri ama kwa sababu sisi ni wafuasi wa kanisa fulani. Kuna njia moja tu ya kuufikia Uzima wa Milele, na hiyo ni kupitia kwa Yesu Kristo. Yeye alituagiza ya kwamba hatuna budi KULIAMINI Neno Lake, ambalo ni Biblia. Vinginevyo, tungewezaje kuokolewa?

Wakati siku ya hukumu itakapowajilia, je! mtasikia, “Njoni, mliobarikiwa na Baba Yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu,” (Mat. 25:34) ama mtasikia, “Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake”? (Mat. 25:41)

Wakati macho yako yakiyapitia maneno haya, una chaguo la kufanya: Je! utachagua kuliamini Neno la Mungu?

Utaishi wapi milele?







Marejeo

Ayubu 14:12-16

Ni vivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke; hata wakati mbingu kutokuwako tena, hawataamka, wala kuamshwa usingizini.

Laiti ungenificha kuzimuni, ukanilinda kwa siri, hata ghadhabu zako zitakapopita, na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka!

Mtu akifa, je! atakuwa hai tena? Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, hata kufunguliwa kwangu kunifikilie.

Wewe ungeita, nami ningekujibu; ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako.

Lakini sasa wazihesabu hatua zangu; Je! huchungulii dhambi yangu?

Ayubu 19:23-26

Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni.

Yakachorwa katika mwamba milele, kwa kalamu ya chuma na risasi.

Lakini mimi ninajua ya kuwa mkombozi wangu yu hai. Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.

Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, bado nikiwa na mwili wangu nitamwona Mungu.

Mathayo 7:21-23

Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.

Mathayo 22:14

Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.

Yohana 3:16-17

Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.

Yohana 5:24

Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.

I Wakorintho 2:9

Lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.

I Wathesalonike 4:13-18

Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumini.

Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye.

Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.

Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.

Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

Basi farijianeni kwa maneno haya.