Mara nyingi Ndugu Branham hutoa sifa za Nguzo ya Moto iliyoithibitisha huduma yake. Ilikuwako alipozaliwa, ilionekana na maelfu ukingoni mwa Mto Ohio, na ilionekana kumfuata kokote alikoenda. Ilikuwa ni mwaka wa 1950 ambapo Bwana aliwapa waaminio na wasioamini vile vile thibitisho lisilokanushika ya kwamba Nguzo hii ya Moto ilikuwa pamoja na nabii huyu.
Usiku huo ulikuwa umegubikwa na ubishi kwenye Jumba Kubwa la Mikutano la Sam Houston. Ndugu Branham alikuwa akiongoza uamsho wa uponyaji uliokuwa ukienea nchini. Baraka za Bwana Yesu zilikuwa zikimiminika kama mvua kwenye mashamba ya ngano ya kiroho. Bali hizo ishara kuu na maajabu hazikutokea bila upinzani. Kama ilivyo kawaida siku zote, adui alimwinua mshindani. Vikosi hivyo viwili vilikutana Houston, Texas, Naye Malaika wa Bwana Mwenyewe akashuka kupiga vita.
Maelfu tayari walikuwako kushuhudia miujiza isiyohesabika iliyomfuata mtu huyu wa Mungu. Siku moja kabla, kundi la wahudumu walimpa changamoto nabii kufanya mjadala juu ya uponyaji wa Kiungu, bali changamoto hiyo ilimwangukia rafiki mzee mwaminifu wa nabii, Kasisi F.F. Bosworth. Hao wenye kushuku wengi waliongozwa na mhudumu wa mahali hapo wa Kibaptisti na ambaye ni mnenaji mkosoaji wa uponyaji wa kiungu. Mjadala huo uliokuwa unakuja ulifichuliwa kwa magazeti, ambayo upesi yalichapisha vichwa vya habari, “Manyoya ya Kitheolojia Yatapeperushwa Saa 1 usiku Wa Leo Katika Jumba Kubwa la Mikutano La Sam Houston.”
Mpinzani alimkodisha mpiga picha mweledi, Ted Kipperman wa Studio za Douglas, apate kunakili mjadala huo kwa picha. Jioni hiyo, picha zilipigwa za Ndugu Bosworth akiwa amesimama kwa ustaha huku huyo mwenye kushuku akiwa katika mikao ya kumtishia; wakati mmoja kidole chake kimekitwa kwenye uso wa mzee huyo mnyenyekevu.
Mjadala huo ulipoanza, Kasisi Bosworth upesi alithibitisha uhakika wa uponyaji wa Kiungu kwa ushuhuda wa Maandiko na halafu, kusudi asiliache swali lo lote, akawaomba wote waliokuwa wameponywa maradhi yao kusimama. Maelfu wakasimama kwa miguu yao. Baada ya hao walioponywa kuketi chini, aliwaomba wale wote waliokuwa wameponywa kwa uponyaji wa Kiungu waliokuwa ni wafuasi wenye sifa njema wa dhehebu la mtu huyu wangesimama. Wafuasi mia tatu wa kanisa hilo wakasimama na kwa fahari wakaonyesha rehema ambayo Bwana Yesu alikuwa amewaonyesha.
Changamoto basi ikatokea kwa huyo mwenye kushuku. “Hebu huyo mponyaji wa Kiungu ajitokeze. Hebu atende kazi.” Ndugu Bosworth akasema wazi ya kwamba Yesu alikuwa Ndiye Mponyaji pekee wa Kiungu, bali kelele za majigambo ya mkosoaji yakaendelea. Hatimaye, Ndugu Bosworth akamwalika Ndugu Branham jukwaani. Akakubali mwaliko huo huku kukiwako na makelele ya shangwe ya kumuunga mkono.
Nabii, huku amejazwa na Roho Mtakatifu, alitoa jibu hili:
Siwezi kumponya mtu yeyote. Nasema jambo hili. Wakati nilipokuwa mtoto mchanga aliyezaliwa katika Mkoa wa Kentucky, kulingana na mama yangu mpendwa, na jambo ambalo limethibitishwa maishani mwangu mwote, kuna Nuru iliyoingia kwenye chumba cha kibanda maskini kile kilichosongamana vitu kule, mahali kilipokuwa, hakijasakafiwa, hata hakikuwa na dirisha, walikuwa tu na maskini kitu fulani cha kale kama dirisha pale, kama kijilango, nao wakakisukuma wakakifungua yapata saa kumi na moja alfajiri, na Nuru hii ikazunguka ikaingia kama wakati tu kukipambazuka. Tangu wakati huo, imekuwa pamoja nami. Ni Malaika wa Mungu. Alikutana nami uso kwa uso miaka michache iliyopita. Kote katika maisha yangu, Yeye aliniambia mambo ambayo yametukia, nami nimeyasimulia tu kama vile alivyoniambia. Nami ninampa changamoto mtu yeyote mahali popote, aende kwenye mji niliolelewa, ama popote pale, ambapo tamshi limepata kutolewa katika Jina la Bwana, ila lile lililotimia vile vile hasa jinsi lilivyosemwa lingekuwa.
Baada ya kusema maneno hayo, Roho Mtakatifu alishuka hapo jukwaani, naye mpiga picha mwenye kusisimkwa akapiga picha. Ndugu Branham aliondoka jukwaani kwa tamshi rahisi, hata hivyo la kinabii: “Mungu atashuhudia. Sitasema zaidi.”
Mwenziwe Bw. Kipperman upesi alienda kuzisafisha picha hizo kwa ajili ya taarifa za habari za kesho yake asubuhi. Aliona kitu cha ajabu alipokuwa akiitoa picha ya kwanza kutoka kwenye mmumunyo wa kusafishia. Hiyo, kama picha zingine tano zilizofuata, ilikuwa ni tupu. Aliushika moyo wake akaanguka kufudifudi wakati alipotoa picha ya mwisho kutoka kwenye mmumunyo huo. Hapo, kwenye picha hiyo ya mwisho, kulikuwako na ile Nguzo ya Moto katika umbo linaloonekana imetulia juu ya kichwa cha nabii wa Mungu, William Marrion Branham.
Wana wa Israeli waliishuhudia ile Nguzo ya Moto ikimwongoza Musa, nao watu wa siku hizi wameishuhudia Nguzo ile ile ya Moto ikimwongoza nabii mwingine.
Picha hiyo upesi ilipelekewa George J. Lacy, Mchunguzi Mweledi wa Hati Zinazoshukiwa wa F.B.I. ya Marekani, ambaye aliihakiki picha hiyo kwa maoni yake ya kitaalamu. Hati rasmi iliyotolewa na Bw. Lacy iko kwenye ukurasa unaofuata.
Hii ilikuwa ni mapema zaidi kabla ya makompyuta na kamera za tarakimu, wala haingeweza kuelezewa kwa njia zozote zinazojulikana na sayansi, mbali na kwamba kulikuwa na Nuru halisi juu ya kichwa cha William Branham. Leo hii picha hiyo hiyo inaweza kuonekana kwenye Maktaba ya Bunge la Marekani, katika makao makuu ya taifa, Washington DC.