KUZURIWA NA MALAIKA



Maono yaliendelea. Aliambiwa na makasisi wenzake ya kwamba maono yake hayakutoka kwa Mungu. Aliambiwa alikuwa amepagawa na roho mchafu. Hili lilimsumbua sana. Mzigo huo ukawa mzito sana asingeweza kuubeba, kwa hiyo akaenda nyikani akayatafute Mapenzi ya Mungu. Alikuwa amejitolea sana hivi kwamba aliapa kutorudi bila jibu. Ilikuwa ni kule, kwenye kibanda cha kale cha kutega wanyama, ndipo Malaika wa Bwana alipompa agizo lake. Miongoni mwa mambo mengine, Malaika huyo alimwambia hivi: “Ukiwafanya watu wakuamini wewe, na uwe mwaminifu unapoomba, hakuna kitakachosimama mbele ya maombi yako, si hata kansa.”

Tashwishi zote ziliondoka. Sasa alikuwa na agizo na kwa ujasiri akajitokeza. Uamsho wa uponyaji ulikuwa umeanza.

Mamia ya maelfu walihudhuria miamsho ya Branham. Maelfu waliponywa katika Jina la Bwana Yesu Kristo. Wainjilisti wengine kama vile Oral Roberts, T.L. Osborn, na A.A. Allen mara wakamfuata Ndugu Branham na kuanzisha miamsho yao wenyewe ya uponyaji. Bwana alizimimina baraka Zake kuliko hapo awali. Mkono wa uponyaji wa Yesu Kristo mara nyingine tena ulikuwa umewagusa watu Wake.

“Mara nyingi nimelia kwa furaha kuhusu karama ya hivi karibuni ya Mungu kwa kanisa la ndugu yetu mpendwa, William Branham, pamoja na karama yake ya ajabu sana ya uponyaji. Hili ni jambo la Mungu kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo (Efe. 3:20), kwa maana kamwe sijapata kuona wala kusoma juu ya chochote kinachofanana na huduma ya uponyaji ya William Branham.”

Kasisi F.F. Bosworth, mwinjilisti anayejulikana ulimwenguni kote na mmoja wa wazee waanzilishi wa dhehebu la Assemblies of God pamoja na mfumo wa siku hizi wa Upentekoste.

“Katika tukio moja, tuliangalia wakati akizungumza na mtu fulani aliyelala kwenye machela. Mwanzoni hakukuwako na ishara yoyote ya jibu la kueleweka kutoka kwa mtu huyo. Baadaye maelezo yalitoka kwa mkewe aliyekuwa amesimama hapo karibu, ya kwamba mtu huyo hakuwa tu akifa kwa kansa, bali alikuwa ni kiziwi wala asingeweza kusikia yaliyokuwa yakisemwa.

Ndugu Branham basi akasema ya kwamba ingefaa mtu huyo kupokea kusikia kwake ili kwamba aweze kumwelezea kuhusu kuponywa kwa kansa yake. Kulikuwa na muda mfupi wa maombi. Mara moja mtu huyo aliweza kusikia! Machozi makubwa makubwa yalitiririka mashavuni mwa mtu huyo ambaye uso wake jioni nzima ulikuwa haushiriki kitu kabisa na haukuonyesha hisia yoyote. Alisikiliza kwa shauku kuu alipokuwa akiambiwa juu ya ukombozi wake kutokana na kansa.”

Kasisi Gordon Lindsay, mwandishi hodari, mhudumu, na mwanzilishi wa Chuo cha Kristo kwa Mataifa Yote.

“Ndugu Branham akasema, ‘Huyo Mbunge ameponywa.’ Moyo wangu ukaruka. Nikapiga hatua nikatoka na kumkubali Bwana kama Mponyaji wangu. Nikaweka kando mikongojo yangu…ndipo upande wa chini wa Mbinguni ukaanguka!”

William D. Upshaw, Mbunge wa Marekani (1919-1927), alipigania Urais wa Marekani katika mwaka wa 1932. Alikuwa ni kiwete tangu alipoanguka akavunja mgongo wake akiwa mtoto. Alikuwa na umri wa miaka 84 wakati alipoponywa kabisa kutokana na maombi ya Ndugu Branham, baada ya kuwa kiwete kwa muda wa miaka 66. Kamwe hakuhitaji tena kiti cha magurudumu ama mikongojo hata mwisho wa maisha yake.

“Nilikuwa nimelala chali kwa muda wa miaka minane na miezi tisa nikiwa na T.B. na madaktari walikwishanikatia tamaa. Hata sikuwa nimefikisha uzito wa ratili 50 na ilionekana kana kwamba matumaini yote yalikuwa yamekwisha. Ndipo kutoka Jeffersonville, Indiana, alikuja Kasisi WM Branham katika ono alilokuwa ameona la mwana-kondoo akiwa ameshikwa kichakani na alikuwa akilia ‘Milltown’, ambako ndiko ninakoishi. Ndugu Branham hakuwa amewahi kuja huku wala kujua mtu yeyote aliyetoka huku. Akiingia, aliweka mikono juu yangu na akaomba, akiliitia juu yangu Jina la Bwana wetu mpenzi Yesu. Kitu fulani kilionekana kunishika na kwa ghafla nilikuwa nimeamka na kumshukuru Mungu kwa nguvu Zake za kuponya. Sasa mimi ni mpiga piano kwenye kanisa la Kibaptisti hapa.”

Georgia Carter, Milltown Indiana, aliponywa ugonjwa wa kufisha wa T.B. mwaka wa 1940 wala kamwe hakuugua ugonjwa huo hata wakati mmoja tena maishani mwake. Anawakilisha makumi elfu ya watu ambao wameponywa kupitia kwa huduma yake na wangali wanaponywa leo.