Yohana 14:12

Amin, amin, nawaambia, Yeye aniaminiye Mimi, kazi nizifanyazo Mimi yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizi atafanya; kwa kuwa Mimi naenda kwa Baba Yangu.


Marko 16:17-18

Na Ishara Hizi Zitafuatana Na Hao Waaminio; Kwa Jina Langu Watatoa Pepo; Watasema Kwa Lugha Mpya;

Watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.


Sisi sote tunaweza kuzifungua kurasa za Biblia na kuona ya kwamba Mungu hutenda miujiza: Musa aliigawanya Bahari ya Shamu, Eliya aliagiza njaa, Yesu alitembea juu ya maji, nao wanafunzi waliwaponya wagonjwa.

Kuna maelfu ya matukio ya kimiujiza yaliyoandikwa katika Biblia. Kama Mungu hushuhudia kwa ishara na maajabu, basi iko wapi miujiza Yake siku hizi? Je! Yeye anaweza kuponya kansa kama alivyoponya ukoma katika Biblia? Vipi kuhusu UKIMWI ama malaria? Je! Yeye angali anaweza kufanya muujiza? Naam, Mungu angali anafanya miujiza na ishara hizi hufuatana na hao waaminio.

Sasa, angalieni enyi marafiki, wazieni juu ya Mfalme George wa Uingereza, wakati alipoponywa ugonjwa mbaya sana wa kushupaa kwa mishipa mwilini, wakati tulipomwombea. Wazieni juu ya Florence Nightingale, (nyanya yake, mwanzilishi wa Red Cross), alikuwa na uzito wa yapata ratili sitini, amelazwa kule akifa kwa kansa kwenye mbuti ya tumbo, amelala kule akifa. Maskini hua mdogo aliruka akaingia kichakani kule na ndipo Roho wa Mungu akaja na kusema, “BWANA ASEMA HIVI, ataishi.” Na ana uzito wa ratili mia moja na hamsini na tano akiwa katika afya nzuri kabisa.

Wazieni juu ya Mbunge Upshaw akiketi hawezi vitini na kitandani mwaka baada ya mwaka, kwa muda wa miaka sitini na sita. Na mara moja papo hapo alisimama kwa miguu yake, akatimua mbio jengoni, akavigusa vidole vyake vya miguu, alipona kikamilifu kabisa na akawa mzima.

Wazieni tu juu ya maelfu na maelfu ya watu ambao wameponywa. Kwa nini tuketi hapa hata tufe? Hebu na tufanye jambo fulani juu yake.

Kuwa na imani kama wewe ni mgonjwa ama ni mhitaji. Biblia inasema ya kwamba Yesu Kristo ni yeye yule jana, na leo, na hata milele, kwa hiyo kama Yeye aliweza kufanya muujiza miaka elfu mbili iliyopita, basi Yeye anaweza kufanya vivyo hivyo leo. Yeye alituahidi ya kwamba tumeponywa, kama tungeamini tu.

Mbunge Upshaw

William D. Upshaw alitumika miaka minane katika Bunge la Uwakilishi la Marekani kisha akagombea kiti cha Urais mwaka wa 1932. Ajali ya kilimo ilimlemaza akiwa mtoto, naye akaishi miaka 66 ama kwenye mikongojo au kwenye kiti cha magurudumu. Katika mwaka wa 1951, aliponywa kabisa na akatembea kikamilifu hata mwisho wa maisha yake.

 
Florence Nightingale

Florence Nightingale, jamaa wa mbali wa yule nesi mashuhuri, alikuwa na ugonjwa wa kansa ya kufisha ya tumboni. Alituma picha hii kama ombi la mwisho la maombi kabla kansa haijayachukua maisha yake. Kama unavyoweza kuona, alikuwa karibu ya kufa kabla Bwana Yesu kumponya mwaka wa 1950. Picha ya pili ilipigwa baada ya kuponywa kwake na kutumwa kama ushuhuda ya kwamba Mungu angali anawaponya wagonjwa.


Tris Griffin

Tris Griffin alienda ofisini kwa daktari mapema mwaka wa 2013 kwa sababu ya kuumwa na mgongo ambako alihofu kungeweza kuwa ni marudio ya vita vyake dhidi ya kansa. Uchunguzi wa MRI ulionyesha “ubainishaji wa mshipa mkubwa wa damu” wa moyo wake, ambao uliwafanya madaktari kumfanyia uchunguzi zaidi na kuandaa upasuaji wa dharura kesho yake. Mstari unaopitia moyoni kwenye picha hii ni ufa dhahiri ambao ungemaanisha kifo cha upesi na karibu cha hakika kama ungepasuka.

Kesho yake baada ya waaminio kumwombea, madaktari walifanya uchunguzi mwingine wa CT kusudi wabaini ulipo hasa huo ufa kabla ya upasuaji. Wakati huu, picha hiyo ilionyesha moyo wenye afya nzuri kabisa. Akiduwaa, daktari huyo alimwambia Bi. Griffin, “Sijui la kukwambia. Ulikuwa na ugonjwa wa kuchanguka kwa mkole lakini sasa dalili zote zimetoweka.” Akamwonyesha zile picha zilizopigwa kabla ya maombi na halafu za baadaye. “Uko huru kwenda, na jambo lingine, hakuna dalili yoyote ya kansa pia. Una afya nzuri kabisa.”

 

Mshale wa daktari umeelekeza kwenye mkole, ambao ni eneo hili jeusi la duara katikati ya picha. Mstari huo wa hanamu unaopitia kwake ndio perema, ama “kuchangua” kwa mkole, ambao unahitaji upasuaji wa mara moja na ni wa kufisha ukipasuka. Uchunguzi wa pili ulifanywa kesho yake. Ule mkole ulitoweka kabisa na kamwe haukurudi.

Marejeo

Zaburi 103:2-3

Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, wala usizisahau fadhili zake zote.

Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote.

Isaya 53:5

Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

Marko 16:17

Na ishara hizi zinafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya.

Luka 17:6

Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii.

Yohana 14:12

Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye Mimi, kazi nizifanyazo Mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa Mimi naenda kwa Baba.

I Wathesalonike 1:5

Ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu.

Waebrania 2:3-4

Sisi je! tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia;

Mungu naye akishuhudu pamoja nao kwa ishara na ajabu, na kwa miujiza mbalimbali na karama za Roho Mtakatifu alizozigawa kulingana na mapenzi Yake.

Waebrania 13:8

Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.

Yakobo 5:15

Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.

I Petro 2:24

Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.