Mwanzo 3:1
Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, ati! Hivi ndivyo alivyosema mungu, msile matunda ya miti yo yote ya bustani?
Mwanzo 3:6-7
Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.
Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.
Mwanzo 3:14-15
BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako.
Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.
Hii ndiyo dhambi ya kwanza iliyoandikwa katika Biblia. Mnyama aliyekuwa mjanja sana kuliko wanyama wote, yule ibilisi, “alimdanganya” Hawa akala kipande cha tunda lililokatazwa. Alikila kisha akampa na mumewe, jambo ambalo liliwafanya kutambua ya kwamba walikuwa uchi.
Maswali dhahiri ni: Nyoka anawezaje kuongea? Tofaa lina uhusiano gani na kuwa uchi? Na, uzao wa nyoka unaingianaje na yote haya?
Biblia inasema nyoka alikuwa “mwerevu” kuliko wanyama wote. Alifanana sana na mwanadamu, hata angeweza kutembea, kuzungumza, na hata kuwa na mazungumzo ya maana. Baada ya kumdanganya mke wa Adamu, Mungu alimlaani awe nyoka, bali si kabla ya uharibifu kufanywa na mbegu kupandwa.
Biblia inasema katika Mwanzo 3:15 ya kwamba nyoka alikuwa na uzao, na Mungu akaweka uadui kati ya asili hizo mbili. Ni dhahiri kwamba, mbegu ya nyoka ilichanganyana na mbegu ya kawaida ya Hawa kabla ya kutenganishwa. Hayo yote yangekuwaje ni matokeo ya kula tofaa? Halafu, vifungu vichache baadaye, “Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.” Angalia ya kwamba halisemi Adamu alikuwa ndiye baba yao wote walio hai.
Kuna “matunda” mbalimbali katika Biblia. Kwa kweli, kuna tunda halisi, kama vile tofaa, ambalo linakua na kuliwa kama chakula. Kuna pia tunda linalomaanisha matendo yetu, kama ni kazi zetu za kawaida kama vile ukulima na biashara, ama kazi za kiroho kama vile kufanya miujiza na kuihubiri Injili. Halafu, kuna tunda la tumbo, ambalo linamaanisha kupata mimba na kuzaa mtoto.
Je! kula tunda la kawaida kungeweza kuwapa Adamu na Hawa ufahamu kwamba walikuwa uchi? Ama, ingechukua uhusiano wa kimwili kati ya mwanamume na mwanamke kwao kufahamu ni kwa nini wanapaswa kufunika sehemu fulani za miili yao?
Ni kitu gani hasa kilichotukia siku ile katika Bustani kuifanya jamii yote ya binadamu kuanguka?
Kama vile Uzao wa mwanamke ulivyokuwa ndiyo njia halisi ya Mungu kujizaa Mwenyewe katika mwili wa kibinadamu, vivyo hivyo uzao wa nyoka ndiyo njia halisi Shetani aliyoona aliweza kujifungulia mlango wa kuingia katika jamii ya kibinadamu. Isingewezekana kwa Shetani (kwa kuwa yeye ni kiumbe tu cha kiroho KILICHOUMBWA) kujizaa kama vile Mungu alivyojizaa, kwa hiyo taarifa ya Mwanzo inaelezea jinsi alivyozaa uzao wake na kujitia ama kujiingiza katika jamii ya kibinadamu. Pia kumbuka ya kwamba Shetani anaitwa “nyoka.” Uzao wake ama kule kujiingiza katika jamii ya kibinadamu ndio tunaozungumzia.
Kabla Adamu hajapata kujuana kimwili na Hawa, yule nyoka alitangulia kujuana naye. Na yule aliyezaliwa kwake alikuwa ni Kaini. Kaini alikuwa ni wa (alizawa, alitokana na) “Yule Mwovu,” (I Yohana 3:12.)
…Ukweli wa mambo ni kwamba Hawa alikuwa na wana WAWILI (mapacha) katika tumbo lake kutokana na kutiwa mimba kuwili MBALIMBALI. Alikuwa amewabeba mapacha, kwa namna fulani mimba ya Kaini ikiitangulia ile ya Habili.
Marejeo
Mwanzo 3:6-7
Mwanamke alipoona ya kwamba ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.
Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.
[Wangejuaje walikuwa uchi kwa kula kipande cha tunda?]
Mwanzo 3:13-15
BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilofanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.
BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako;
Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.
[Huyo nyoka alikuwa na uzao. Ni dhahiri, hili halineni juu ya nyoka.]
Mwanzo 3:20
Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.
[Kwa nini Adamu haitwi baba yao wote walio hai?]
Mwanzo 4:1-2
Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa BWANA.
Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.
[Uhai wote hutoka kwa Mungu, kama umezaliwa kihalali ama si halali. Shetani hawezi kuumba uhai.]
Luka 3:38
Wa Enoshi, wa Sethi, wa Adamu, wa Mungu.
[Yu wapi Kaini mzaliwa wa kwanza kwenye ukoo wa Adamu?]
I Yohana 3:12
Si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.
[Mungu alimuumba Adamu katika mfano Wake Mwenyewe. Je! uovu wa Kaini ulitoka wapi, na haki ya Habili ilitoka wapi? Walirithi sifa zao kutoka kwa baba zao.]
Yuda 1:14
Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake maelfu maelfu.
[Hakuna mahali popote katika Biblia ambapo Kaini yuko kwenye ukoo wa Adamu.]